WANAWAKE kwa muda mrefu wamekuwa wakiaswa kujituma na kujiamini ili waweze kufanikiwa katika kutimiza ndoto zao.
Kujiamini huko kunaweza kuwa na manufaa mengi katika kuinua maisha ya wanajamii hasa kama mhusika atakuwa akijiamini na kuanzisha mradi wake wa kujiajiri na kujikuta akiajiri watu wengine wengi. Zainab Ansell, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Utalii ya Zara ni miongoni mwa wanawake waliojitoa mhanga, kwa kuacha ajira na kuamua kujiajiri.
Kwa kuwa alikuwa na malengo, Zainab amefanikiwa si kujiajiri kwa mafanikio tu, bali pia ameweza kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania, hususan vijana.
Kwa Zainab, mzaliwa wa Hedaru, Same mkoani Kilimanjaro awali alikuwa ameajiriwa na Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), mnamo mwaka 1984 akiwa kitengo cha kukata tiketi za ndege za shirika hilo ambalo kwa sasa liko taabani kiuchumi.
Miaka miwili baada ya kuajiriwa, mama huyo aliyezaliwa mwaka 1959 aliamua kuingia rasmi katika ujasiriamali.
Lakini leo hii, ikiwa ni miaka 25 tangu achukue uamuzi wa kujiajiri, Zainab hana cha kujutia, zaidi ya kujipongeza kwa mafanikio yaliyovuka milima na mabonde, kiasi cha kuwa mwanamke wa kupigiwa mfano.
Na haikushangaza kuona mwaka huu akitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Mwanamke Bora Mjasiriamali katika tuzo za Mwanamke Bora zilizoandaliwa na Kampuni ya Frontline ya jijini Dar es Salaam.
Mafanikio yake yametokana na kupanuka kwa biashara zake kwa kiasi kikubwa, sasa akiwa anamiliki kampuni kubwa ya utalii, ikiwa na hoteli tano za kitalii, kwa ujumla akiwa na zaidi ya wafanyakazi 9,000!
Katika mazungumzo na HABARILEO Jumapili, Zainab anasema kuwa tangu alipoamua kujiajiri, alilenga kujituma ili aweze kutimiza ndoto ya kuwa mwajiri na mmiliki wa vivutio vya utalii nchini.
Akizungumzia alivyoanza biashara, anasema kuwa mwaka 1986 akiwa katika ofisi za Air Tanzania aliingiwa na shauku ya kuwa anasimamia safari za watalii wake mwenyewe huku akiwakatia tiketi na kuwapeleka Mlima Kilimanjaro na kwingineko kwa shughuli za kitalii.
Anakumbuka wakati huo alikuwa na umri wa miaka 27 tu (sasa ana umri wa miaka 52), alifunguka macho na kuamua kufungua ofisi yake katika eneo la Hoteli ya Moshi ambapo alikuwa na wafanyakazi watatu mwaka huo.
Anasema kwamba, alianza katika mazingira magumu, akivizia watalii katika kituo cha mabasi na kuwashawishi kwenda kupanda Mlima Kilimanjaro chini ya kampuni yake, huku akisisitiza kuwa, siri kubwa ya kuwamudu wateja hao ilikuwa ni kauli nzuri na kuwa mchangamfu.
“Ni kwamba kila kukicha nilikuwa najipangia mikakati mipya juu ya nini nifanye ili niweze kuinuka na kusaidia jamii inayonizunguka na ndipo nikajikuta naona umuhimu wa kuwa na hata hoteli za kuwasaidia watalii wanaotumia huduma za kampuni yangu,” anasema Zainab. Ndoto yake ya kuanzisha hoteli ilitimia mwaka 1996, yaani miaka kumi tangu alipoanzisha kampuni.
“Kwa muda mrefu nilikuwa nikiwapeleka watalii wa kampuni yangu katika hoteli mbalimbali kwa ajili ya malazi, kufikia mwaka 1996 nilianzisha hoteli yangu,” anakumbuka mama huyo anayefichua kwamba, hoteli yake ilianza ikiwa na chumba kimoja tu, ingawa kwa sasa ni moja ya hoteli kubwa mjini Moshi.
Inaitwa Spring Land Hotel, sasa ikiwa na zaidi ya vyumba 100 vya kulala, sehemu za kulia chakula, baa moja, bwawa la kuogelea, sehemu ya kuangalia runinga. Pia hoteli hiyo kwa sasa ina bustani zaidi ya nne za kupumzikia, sehemu ya kuchua mwili (massage), sehemu ya mazoezi na sehemu ya kupata joto hasa wakati wa baridi (sauna).
Anasema baada ya kuanzisha hoteli hiyo, ilimwezesha kutoa huduma za kiutalii vyema zaidi kama vile utalii wa kwenda msituni kutembea, utalii wa Moshi mjini kwa baiskeli, kwenda Masai Boma, Marangu na shughuli nyingine muhimu.
Katika kufanikisha ndoto hiyo ya kuwahudumia watalii ameweza kufungua huduma za hoteli zake sehemu nyingine nyingi kama vile Serengeti Wild Camp iliyopo ndani Mbuga ya Serengeti, Ngorongoro Wild Camp iliyopo ndani ya Mbuga ya Ngorongoro na High View Hotel iliyopo katika eneo la Karatu.
Akizungumzia wito wake kwa Serikali kuhusu kuwasaidia wanawake katika kuendeleza utalii anasema kuwa inatakiwa Serikali kuwapa kipaumbele wanawake waliowekeza katika sekta ya utalii kwa kuwapatia maeneo ya kujenga hoteli.
Anasema kuwa kwa kumwezesha mwanamke kuwekeza katika sekta ya hoteli kutasaidia kuendeleza jamii inayozunguka katika maeneo ya hoteli ambapo anatolea mfano wa kampuni yake ilivyoanzisha Taasisi ya kusaidia jamiii iitwayo Zara. Anasema kuwa kupitia taasisi hiyo ameweza kuwasaidia watoto wengi kwa kuwapatia elimu, na huduma nyingine muhimu za afya na za kiroho.
Pia ni mwanzilishi wa Chama cha Wabeba Mizigo wa Wapanda Mlima Kilimanjaro ambapo kupitia chama hicho vijana zaidi ya 3,000 wanapata elimu, mikopo pamoja na misaada mbalimbali ya kijamii. Chama hicho alichokianzisha kwa sasa kinatambulika kimataifa kwa kuwa kupitia wabeba mizigo hao, watalii wengi wameweza kupitishia michango yao na kuifikia jamii.
Anasema kuwa asilimia moja ya fedha anazolipwa mbeba mizigo ya watalii inawekwa katika chama hicho na mwisho wa siku hutumika kuwasaidia wanajamii pamoja na wao wabeba mizigo wenyewe.
“Huruma tuliyonayo wanawake inatufanya kuwa na hali ya huruma ya kutaka kuona jamii ituzungukayo ikiendelea zaidi hivyo tukiwezeshwa kumiliki rasilimali kutatufanya kuisaidia jamii yetu kwa hali na mali hasa kwa kuwapatia mahitaji muhimu” anasema Zara.
Anasema kuwa licha ya kupatiwa tuzo ya kuwa mwanamke mjasiriamali bora wa mwaka, lakini pia ameweza kupatiwa tuzo ya kutambuliwa mchango wake katika sekta ya utalii iliyotolewa nchini Hispania na taasisi ya Bonestor iliyowahusisha akinamama wengine wawili mmoja akitokea nchini Senegal na mwingine Msumbiji.
Pia amewahi kupata tuzo kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) yenye kutambua mchango wake katika masuala ya kijamii. Zainab, mama wa watoto wawili, mmoja akiwa ni meneja wa hoteli yake iliyopo Karatu nje kidogo ya Mbuga ya Ngorongoro anaitwa Leyla na mwingine Anna yuko masomoni Sweden. Anapendelea kuangalia vipindi vya utalii na mazingira katika runinga, huku akiwa anapendelea zaidi kula vyakula vya asili anapenda michezo hasa riadha.
Akizungumzia tuzo ya Zainab ambaye kampuni yake ina mtandao mkubwa wa ofisi ndani na nje ya Afrika, Mkurugenzi wa Kampuni ya Frontline iliyomzawadia mama huyo, Irene Kiwia anasema Zara ni mfano wa kuigwa na kuwa Mkurugenzi wake, Zainab amewafumbua macho akinamama wengi katika kuthubutu. Anasema kuwa, Zainab anaweza kutumiwa kama mfano katika kuwapatia moyo wasichana wadogo hasa wa sekondari na vyuo kwa kuwaonesha ni kwa jinsi gani wanaweza kufanikiwa hasa wakijiamini na kuwa na malengo. “Binafsi naona kuwa huyu mama ni mfano na ndio maana ameweza kutunukiwa tuzo hii kwa kuwa ameweza kutoka chini kabisa hadi kufika juu kiasi cha hata kuajiri wafanyakazi wengi, karibu 10,000! Jiulize, mtu alikuwa ameajiriwa, leo hii anafanya mambo makubwa hivi, kwanini umuhimu wake usitambuliwe? Kwetu sisi, huyu ni mfano mzuri na wa kuigwa,” anasema Kiwia. Huyu ndiye Zainab Ansell, mama mcheshi na mchapakazi ambaye alithubutu kuanzisha kitu chake, akakisimamia, na leo hii anawaacha wengi midomo wazi kutokana na hatua kubwa aliyofikia kimaisha, kibiashara na pia katika kuisaidia jamii na Serikali katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana. Ama kweli, Zainab ni mfano wa kuigwa na miongoni mwa nyota wa kweli katika Tanzania ya leo.
Source : HabariLeo