Home

HOME I

Sunday, April 3, 2011

Historia ya Gaddafi

 

Kanali Muammar Gaddafi ni kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika na katika nchi za Kiarabu.
Gaddafi
Gaddafi

Ameongoza Libya tangu alipompindua Mfalme Idris I, katika mapinduzi yasiyo ya kumwaga damu, wakati huo akiwa na umri wa miaka 27.
Maarufu kwa nguo anazopenda kuvaa, na walinzi wa kike wenye kubeba silaha, kiongozi huyo wa Libya pia anadhaniwa kuwa na mbinu nzuri za kisiasa, kwa kuweza kuirejesha Libya kutokana na kutengwa kidiplomasia duniani.
Baada ya miongo miwili ya kutengwa katika jamii ya kimataifa, mwaka 2003, Tripoli ilikiri kuwa walifanya shambulio la Lockerbie kwa kuiangamiza kwa mabomu ndege ya Pam Am na hapo Umoja wa Mataifa ukaondoa vikwazo dhidi ya Libya.
Gaddafi mwaka 1969
Gaddafi mwaka 1969

Baada ya miezi kadhaa, serikali ya Kanali Gaddafi ilisitisha mipango yake ya kuunda silaha za maangamizi na hii ikarejesha ushirikiano na nchi za magharibi.
Hapo ndipo mabadiliko halisi yalionekana kwa kuwa nchi hizo za magharibi zilibadili mtazamo wao na kuacha kumtenga Gaddafi na kushirikiana naye hata kama alikuwa hatabiriki.
Ni mtu wa kipekee katika kauli zake, mienendo yake, tabia zake na mikakati yake, kwa mujibu wa Saas Djebbar mtaalam wa siasa za Libya.
'Lakini ni mwanasiasa mashuhuri; hakuna shaka lolote kuhusu hilo. Ni mwanasiasa anayeweza kuhimili misukosuko ya kisiasa kwa hali ya juu sana.'

Asili ya Mabedui

Muammar Gaddafi alizaliwa jangwani karibu na Sirte mwaka 1942.
Gaddafi katika mkutano Sirte
Gaddafi katika mkutano Sirte

Alipokuwa kijana alivutiwa na kiongozi mzalendo wa Misri na, Gamal Abdel Nasser, alipokuwa akishiriki katika maandamano dhidi ya Israel wakati wa mtafaruku wa Suez mwaka 1956.
Gaddafi alipanga njama ya kupindua utawala wa kifalme alipokuwa mwanafunzi wa kijeshi na aliwahi kupata mafunzo zaidi akiwa Uingereza kabla ya kurejea nyumbani Libya, mji wa Benghazi, na kupanga mapinduzi ya tarehe 1 Septemba mwaka wa 1969.
Ghaddafi alianza kujenga itikadi zake za kisiasa mwaka 1970 na kuziandika katika kitabu chake cha kijani kibichi.
Gaddafi alipokuwa akizuru Senegal mwaka 1985
Gaddafi alipokuwa akizuru Senegal mwaka 1985

Alikitumia kitabu chake kuanzisha mfumo wa kisiasa iliyojumuisha kanuni za kiislamu na mfumo uliyo tofauti na siasa za ujamaa au ubepari.
Mwaka1977 aliasisi mfumo ujulikanao kama 'Jamahiriya' au 'Taifa la Umma' ambapo raia ndio wanaoendesha uongozi wa nchi yao kupitia 'kamati za umma'.
Hema ya Gaddafi
Hema ya Gaddafi

Mfumo huo wa Gaddafi umevuka mipaka na hauhusishi mambo ya siasa tu, bali pia mambo mengine.
Akiwa safarini ng'ambo, huwa anakaa kwenye kambi iliyojengwa na hema yake ya kifahari ya Kibeduwi akiwa amefuatana na walinzi wanawake ambao, inasemekana, huwa hawapotezi umakini kazini kama walinzi wanaume.
Hema hiyo pia hutumiwa kuwalaki wageni wa Libya na Kanali Gaddafi huendesha mikutano na mahojiano yake humo humo akipepea usinga au tawi la mitende.

Upekepeke

Benjamin Barber, mtaalam wa kisiasa wa kujitegemea, kutoka Marekani amewahi kukutana na Gaddafi mara kadhaa hivi karibuni na kuzungumza naye kuhusu mustakabali wa Libya.
Gaddafi akiwa na viongozi wengine wa nchi za Uarabuni
Gaddafi akiwa na viongozi wengine wa nchi za Uarabuni

Bw Barber alisema kuwa Muammar Gaddafi anajihisi kuwa msomi aliyebobea.
Muammar Gaddafi na Tony Blair waliwahi kuandaa mkutano wa viongozi kutoka nchi mbalimbali tarehe 29 Mei 2007 kwenye hema hiyo ya Kibedui.
"Utashangazwa kuwa ingawaje ni dikteta, ni mwanafalasafa na mwenye kutafakari jambo kabla ya kuzungumza," aliiambia BBC.
"Namchukulia sana kama mtu kutoka kabila la Waberber na mtu ambaye aliibuka kutoka tamaduni za watu wa jangwani, kutoka kwenye mchanga na kwa namna fulani kuna tofauti kubwa na uongozi wa kisasa, na kwa namna fulani hilo limemfanay awe mstahamilivu na mwenye msimamo."
Kanali Gaddafi amejitahidi kwa muda mrefu kutoa ushawishi wake nyumbani na ng'ambo.
Awali alituma jeshi lake nchini Chad ambapo wanajeshi walidhibiti ukanda wa Aozou, kaskazini mwa nchi hiyo, mwaka 1973.
Katika miaka ya 80 aliandaa mafunzo kwa makundi ya waasi kutoka Afrika Magharibi yaliyojumuisha wale wa Tuareg ambao ni Waberber.
Hivi karibuni aliongoza jitihada za kuwapatanisha waasi wa Tuareg kutoka nchi za Niger na Mali.

'Mbwa kichaa'

Jumuiya ya wanadiplomasia kuitenga Libya kulitokana na Kanali Muammar Gaddafi kuunga mkono makundi yeneye silaha, ikiwemo Irish Republican Army na Palestine Liberation Organisation.
Gaddafi akiwa na mwandishi wa habari wa BBC
Gaddafi akiwa na mwandishi wa habari wa BBC

Rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan alimwita Gaddafi 'mad dog' yaani 'mbwa kichaa' na Marekani ililipiza kisasi dhidi ya Libya kwa madai ya kuhusika na mashambulio ya anga barani Ulaya kwa kuvamia miji ya Tripoli na Benghazi mwaka 1986.
Ilisemekana kuwa Kanali Gaddafi alitikiswa na mashambulio ya mabomu hayo ambapo mtoto wake wa kike wa kufikia aliuawa.
Aliposhindwa katika jitihada zake za kuzipatanisha nchi za Uarabuni katika miaka ya 90, Kanali Gaddafi alielekeza nguvu zake barani Afrika na kupendekeza 'Muungano wa Nchi' za bara la Afrika.
Muuguzi wa Gaddafi
Muuguzi wa Gaddafi

Alianza kuvaa mavazi yake binafsi, sare za michezo zilizo na ngao za bara la Afrika au picha za viongozi kutoka bara hilo.
Wakati wa mabadiliko katika karne ya 20, huku Libya ikiwa inapata tabu kutokana na vikwazo dhidi ya nchi hiyo, alianza kurekebisha hali nchini mwake.
Mwaka wa 2003, mabadiliko yakaanza kuonekana na baada ya miaka mitano mkataba wa kulipa fidia kwa waathirika wa Lockerbire uliafikiwa na hii ikarejesha uhusiano kati ya Washington na Libya.
'Hakutakuwa na vita tena, mashambulio, na vitendo vya ugaidi' Kanali Gaddafi alisema alipokuwa akiiherehekea miaka 39 aliyokaa madarakani.

Changamoto za ndani


Kiongozi huyo wa Libya hujiona kama kiongozi wa kidini wa taifa hilo, akihakikisha kwa kile anachosema ni demokrasia.
Waandamanaji wa hivi karibuni Libya
Waandamanaji wa hivi karibuni Libya

Lakini katika hali halisi, wakosoaji wanasema Kanali Gaddafi amefanikiwa kudhibiti nchi hiyo.
Wanaompinga wamekandamizwa kikatili na vyombo vya habari vinabaki katika udhibiti mkubwa wa serikali.
Libya ina sheria ambazo haziwaruhusi watu kukusanyika katika misingi ya kisiasa zinazopinga mapinduzi ya Kanali Gaddafi.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema serikali hiyo imewatia mbaroni mamia ya raia kwa kukiuka sheria hiyo na baadhi yao kuhukumiwa kifo.
Imeripotiwa kumekuwa na matukio ya utesaji na hata watu kupotea
Inadhaniwa kuwa Kanali Gaddafi anaandaa namna ya kukabidhi madaraka yake kwasababu ya umri aliyofikia sasa lakini haijulikani ni nani atakayerithi uongozi wa Libya kutoka kwa Gaddafi.
Sayf akiwa na ndugu yake Saad
Sayf akiwa na ndugu yake Saad

Kuna hisia kuwa mwanawe Sayf Al-Islam Gaddafi ndiye atarithi uongozi kutoka kwa baba yake na anaongoza katika kuleta mabadiliko.
Ingawaje Sayf ametangaza kuwa anastaafu siasa lakini kuna wanaohisi kuwa hii ni mbinu ya kuongeza ushawishi wake kisiasa.
Wakati huo huo, Gaddafi ameahidi kuwa wizara za nchi hiyo zitafutwa pamoja na bajeti zao
Utajiri utakaopatikana kutokana na mafuta utakabidhiwa moja kwa moja kwa wananchi.
Licha ya uchumi wa Libya kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje, mabadiliko bado yanakwenda taratibu.
Waandamanaji wakichana picha ya Gaddafi
Waandamanaji wakichana picha ya Gaddafi

Walibya wengi wana wasiwasi juu ya mabadiliko yanayotokea na kuhisi kuwa hawapati manufaa kutoka rasilmali ya Libya, waangalizi wanasema kwani huduma za serikali ni duni pamoja na ubadhirifu mkubwa wa mali.
' Wanajihadhari sana katika mapambano hayo kwa kuwa hawataki mabadiliko yatakayolegeza nguvu za umma,' alisema Saad Djebbar
'Lakini wakati huo huo, Walibya wanafahamu kuwa wanahitaji kufanya mabadilko. Na ndio maana wanaenda taratibu sana.
Mfuasi wa Gaddafi
Mfuasi wa Gaddafi

                                                  Chanzo : www.bbc.co.uk/swahili

SUSAN MASHIBE; Rubani, Mhandisi wa Ndege gumzo Afrika Mashariki


Image

Mashibe ni Rubani, Mhandisi wa masuala ya ndege na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni mbili zinazoshughulika na masuala ya anga, lakini unapokutana naye kwa mara ya kwanza huwezi kuamini kama mwanadada huyo ana sifa hizo ndio maana nikakumbuka ule usemi, ‘usitathmini kitabu kwa kuangalia jalada lake.’

Kuthibitisha uwezo wake mkubwa katika fani hiyo, hivi karibuni Mashibe alichaguliwa na Taasisi ya World Economic Forum (WEF) kuingia katika kundi dogo la heshima la vijana waliothibitisha vipaji vya uongozi la Viongozi Vijana Duniani (Young Global Leader- YGL)) kwa mwaka huu wa 2011.

Sambamba na Susan, Mtanzania mwingine Elsie Kanza, Mshauri wa Uchumi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete amechaguliwa na taasisi hiyo pia kuingia katika kundi hilo.

Mashibe na Kanza walichaguliwa kutoka miongoni mwa viongozi vijana 5,000 waliopendekezwa kutoka duniani pote na hatimaye kupitishwa katika mchujo na kuchaguliwa kwenye mchujo mkali na Kamati Maalumu chini ya uenyekiti wa Malkia Rania Al Abdullah wa Ufalme wa Hashemite wa Jordan.

Susan ndiye Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Kampuni ya TanJet, kampuni ya ya kimataifa na ya kwanza ya aina yake nchini inayoshughulikia masuala ya kiufundi katika ndege binafsi, za biashara na hata za kidiplomasia.

TanJet imebadilisha namna biashara ya huduma ya anga inavyoweza kufanya kazi Afrika Mshariki na miongoni mwa wateja wake ni viongozi wa nchi mbalimbali, wafalme, watendaji, watu maarufu na ndege za kijeshi.

Mwanadada huyu pia anamiliki kampuni nyingine inayojulikana kama Kilimanjaro Aviation Logistic Center, ambayo inashughulikia taratibu za utuaji na urukaji wa ndege binafsi katika Bara la Afrika.

Aidha, ameanzisha Huduma ya Matengenezo na Ukarabati wa Ndege Kilimanjaro kwa lengo la kutoa huduma za kisasa, yenye kiwango na salama katika usafiri wa anga wa jumla na ushirika katika eneo la Afrika.

Lakini pia Susan ndiye mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki mwenye Cheti cha Rubani cha FAA na Mhandisi Matengenezo wa Ndege. Tangu kuanzisha TanJet mwaka 2003, Mashibe ametunukiwa Tuzo mbalimbali ikiwemo ya Askofu Desmond Tutu ya mwaka 2009 na ile ya Mwanamke Mjasiriamali mwenye Mafanikio ya mwaka 2009.

Susan anajisikiaje kwa kuwa mtu pekee nchini ambaye ni Rubani na Mhandisi wa Ndege? Hasiti kutoa maoni yake kwani anasema “ najisikia kawaida tu. Sipendi sifa hizi zote…ninachotaka ni kuhamasisha vijana kupitia hadithi yangu ili nao watimize ndoto zao na wasikubali kitu chochote kiwakatishe tamaa.”

Ndoto ya Susan ya kutaka kurusha ndege haikuanza wakati akiwa chuoni la hasha! bali akiwa na umri wa miaka minne tu ndipo alipogundua sehemu inayomfaa ni kwenye `mawingu’. Anasema,“ nilizoea kuwaona wazazi wangu na ndugu zangu wakipanda ndege na kuondoka, wakiniacha.

Wakati huo tulikuwa tukikaa Kigoma na walikuwa wakirudi Dar es Salaam, na niliachwa na bibi. “Nilipokuwa nikiangalia ndege ikiondoka nikawa nafikiria kama ningekuwa najua kurusha ndege nisingeachwa tena,” anasema Susan ambaye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto sita.

Wakati huo wote, Susan alikuwa na shauku kufahamu ni kitu gani cha kufanya ili mtu awe rubani, na kufahamu namna ndege inavyofanya kazi. Anaendelea kusema kuwa, “bado nakumbuka hisia nilizopata nilipoona Ndege ya Shirika la Ndege ya Uingereza aina ya Boeing 737 kwa mara ya kwanza, nilikosa maneno ya kusema, nilikuwa sijaona kitu kizuri na kikubwa kama kile, lakini kilichonivutia zaidi ni namna ndege inavyoanza kuruka.”

Hisia alizopata Susan ziligeuka kuwa mapenzi na kitu cha kuvutia ambavyo vilimtawala binti huyo tangu akiwa mdogo. Mapenzi yake yalitimizwa zaidi pale mjomba wake alipompeleka kwenda kutembea uwanja wa ndege wakati alipokwenda Dar es Salaam kumtembelea akiwa na umri wa miaka 10.

Kila mtu katika familia yake alifahamu malengo ya binti huyo. Kwa hiyo haikuwa kazi ngumu kwa Susan kumshawishi baba kubariki kazi aliyoichagua baada ya kumaliza Kidato cha Nne. “Nilichaguliwa kujiunga na ualimu, lakini baba aliyekuwa mfanyakazi wa umma aliniuliza nataka kufanya nini. Nikamwambia nataka kuwa Rubani, kisha akaniambia timiza ndoto yako.”

Hivyo kweli Susan ametimiza ndoto yake. Mwaka 1993 alianza kozi ya Uhandisi wa Ndege katika Chuo cha South Western Michigan nchini Marekani ambapo dada yake alikuwa akiishi. Baba yake alimshauri kuchukua kozi hiyo nchini Marekani na alilazimika pia kujifunza lugha ya Kiingereza.

“Niliambiwa siwezi kuwa rubani kama sizungumzi Kiingereza kwa sababu nitatakiwa kuwasiliana na mnara wa kuongozea ndege,” anasema. Hata hivyo, mwaka 1995 mambo yalikuwa magumu baada ya familia yake nyumbani Tanzania kusema haiwezi kumsaidia kielimu kutokana na matatizo ya kifedha.

“Kwa muda nilifikiria ndoto yangu imekufa…nilipoteza matumaini, hamu ya kula na matokeo yake niliumwa.” “Nililazwa hospitalini na wakalazimika kunirudisha nyumbani ili nipate nguvu, jambo ambalo nilifanya. Lakini nikiwa nyumbani nilitafuta ufumbuzi wa muda mrefu kuwa kuanzia sasa sitamtegemea mtu ila mimi mwenyewe, niliamua nitarudi kumaliza shule na nitarusha ndege mwenyewe.”

Hicho ndicho alichofanya. Kwa namna fulani alirudia hatua zake na kurudi shule na alihitimu mwaka 1996. Mwajiri wake wa kwanza ilikuwa Kampuni ya Duncan Aviation, iliyokuwa mjini Michigan, Marekani. Susan alianza kazi ya ukaguzi mkubwa katika ndege kadhaa za kibiashara.

“Nilianza masomo ya kurusha ndege katika Chuo Kikuu cha Western Michigan, nikisimamia zaidi katika ndege. Ilikuwa gharama kubwa, na nililazimika kufanya kazi saa nyingi usiku ili niweze kuhudhuria darasa, “ anasema.

Lakini bahati nzuri alikuwa akichukua masomo katika kampuni yake kwa hiyo alilipa nusu ya ada, faida ambayo mwajiri alikuwa akitoa kwa wafanyakazi wake. Mwaka 2002, Susan alipata cheti cha kutambuliwa kufanya kazi katika ndege za biashara, baada ya kumaliza Shahada ya Kwanza ya Utawala wa Mambo ya Anga.

Hata hivyo, maisha yalianza kuwa magumu kwa yeyote aliyeko katika biashara ya ndege kwa sababu ya tukio la mashambulizi ya kigaidi Septemba 11, 2001 nchini Marekani. “Baada ya tukio la Septemba 11, mashirika ya ndege yalipata misukosuko, watu walikosa huduma.

Ilikuwa kazi ngumu, baadhi ya kampuni zilifungwa, kwa hiyo nikaamua nyumbani ndipo natakiwa kuwepo,” anasema. Susan alishajinyima sana na kuweka akiba ya kutosha kurudi nayo nyumbani kwa ajili ya kuanzisha biashara yake.

Kwanza alifikiria kutafuta ajira, lakini kampuni nyumbani Tanzania zilisema elimu yake iko juu sana. Hakuwa na chaguo lingine zaidi ya kutumia akiba yake na kukodi chumba chenye ukubwa wa mita za mraba 13 tu katika Uwanja wa Ndege ambapo alifungua kampuni yake Julai 1, 2007.

“Kila mtu alidharau uamuzi wangu, wakiniambia muda wa miezi mitatu tu nitakuwa nimefunga ofisi, lakini nipo mpaka leo,” anasema na kueleza namna biashara yake inavyolipa. Mteja wake wa kwanza alikuja siku 20 baada ya kufungua biashara yake na alikuwa Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ambaye alifika kutembelea Tanzania.

Washirika wake walioko Afrika Kusini walimuunganisha na kazi ya kuhudumia ndege ya Zuma. Ilikuwa ni hatua kubwa kwake kupata tenda hiyo ya kusimamia ndege zote zilizopo chini ya Ubalozi wa Marekani.

Wakati akifurahia mafanikio hayo makubwa, Susan anasema furaha yake ilikuwa alipoweza kulipa kodi inayofikia kiasi cha Sh milioni 500 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ulikuwa mchango mkubwa uliowashtua wengi. Kama ilivyo kwa wanawake wengi wanapofanya kazi zilizotawaliwa na wanaume zaidi naye amekumbana na vikwazo.

Baadhi ya watu walidharau kwa kumuangalia tu. Anakumbuka aliwahi kuzuiwa kuingia katika ndege ya kidiplomasia kwa sababu walinzi walidhani hana shughuli ya kumuingiza humo. Lakini baadaye walishtuka walipobaini kuwa mwanadada huyo ndio alipewa jukumu la kusimamia ndege hiyo.

“Mimi ni mwanamke, navaa viatu virefu, napaka vipodozi na mambo mengine kama hayo, kwa hiyo rubani anapoangalia na kuona mimi ndiye ninafanya kazi ya kuhudumia ndege yao hushtuka na kudhani sina uwezo huo, wengine hunisimamia ninapofanya kazi, lakini sura zao hubadilika wanapobaini ninachoweza kufanya,” anasema.

Huyo ndiye Susan Mashibe, Rubani na Mhandisi wa Ndege mwenye umri wa miaka 37 ambaye baada ya kujichimbia Marekani akisoma na kupata ujuzi kuhusiana na urubani na uhandisi wa ndege, ameweza kutimiza ndoto yake ya utoto na kukataa kuruhusu vikwazo na kukatishwa tamaa.



                                      Source : HabariLeo