Home

HOME I

Saturday, September 18, 2010

Mfumo mpya: Bila 40,000 hupati leseni ya udereva

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha amezindua utoaji wa leseni mpya za udereva utakaokamilika Julai 30, mwakani na kugharimu Dola milioni 17.25 (zaidi ya Sh bilioni 17) huku leseni moja ikiuzwa kwa Sh 40,000.

Aidha Masha alisema Serikali haitavumilia wala kuwaonea huruma watendaji watakaofanya makosa kwa uzembe au kwa makusudi kwa kuongozwa na maslahi yao binafsi kwa kutoa leseni hizo kinyume cha sheria.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Dar es Salaam jana, Masha alisema serikali iliamua kuanzisha mfumo huo mpya wa utoaji leseni kama sehemu ya mkakati wake wa kupunguza ajali za barabarani pamoja na kuongeza wigo na udhibiti wa mapato ya serikali.

Alisema wale wenye leseni daraja C na hawaendeshi malori, gari za abiria au sifa zinazoendana na daraja hilo ambao huendesha magari yao binafsi wanatakiwa kubadilisha na kupewa leseni ya Daraja D na kusema tayari kuna Vituo tisa vilivyokamilika kuanza kutoa leseni hizo.

Masha alisema ili kupunguza ajali za barabarani, msisitizo umewekwa katika viwango na umahiri wa dereva wakati wa utoaji leseni ili kutimiza azima hiyo madaraja ya leseni yameongezeka hadi kumi na nne ambapo upatikanaji wa kila daraja utategemea uwezo wa dereva pamoja na umahiri aliouonyesha katika mafunzo wakati wa kutahiniwa,” alisema Masha.

Alisema ili kuwawezesha kusimamia kikamilifu mfumo huo, serikali itatoa mafunzo kwa watendaji wa Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato ambao aliwataka kuwa na uzalendo na ushirikiano katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo huku serikali ikiwa na imani ya mfumo huo kuondoa tatizo la kughushi leseni na upatikanaji kinyume cha taratibu.

Alisisitiza kuwa katika mfumo wa zamani ilikuwa vigumu kudhibiti kughushiwa lakini katika mfumo huu mpya kuna mambo mengi hayawezi kughushiwa hata ukibadilisha jina au kunyang'anywa leseni ni vigumu kuchukua nyingine kutokana na kuchukuliwa kwa alama za vidole “ili kuondoa msongamano katika upatikanaji wa leseni hizi, madereva wenye leseni ambazo si daraja C watabadilishiwa pale leseni zao wanazotumia sasa zitakwisha muda wake wa matumizi, napenda pia kusisitiza kuwa leseni za zamani zitaendelea kutumika sambamba na mpya,” alisema Masha.

Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya alisema utoaji wa leseni hizo mpya unafanywa na kampuni ya Israel ya OTI LR Group of nje ya nchi iliyopatikana kwa mujibu wa sheria ya Manunuzi ya Umma na kugharimu zaidi ya Sh bilioni 17 fedha ambazo walikubaliana kuwa watatoa wao na kurudisha kwa muda wa miaka mitatu kwa kutoa leseni moja kwa Sh 40,000.

 
     

No comments: