| | | | | | | | | | | | | | | |
|
|
|
KIJANA Mussa Doto wa Kijiji cha Chabulongo katika Kata ya Kasamwa wilayani Geita, ametimiza azma yake kwa kusafiri kwa baiskeli kutoka Geita hadi Dar es Salaam kwa nia ya kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.
Hata hivyo, Dotto alipofika Singida, Katibu wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi wa Mkoa huo, alimshauri apande basi hadi Dar es Salaam, ndipo jana alitimiza azma yake ya kumsalimia na kumpongeza Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alimpokea kijana huyo wa Kitanzania jana asubuhi Ikulu.
“Rais Kikwete amemshukuru kijana huyo kwa moyo wake huo na kuahidi kumsaidia zaidi katika shughuli zake za kilimo ili apate manufaa na mafanikio zaidi,” ilieleza taarifa ya Ikulu.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete yuko jijini Arusha kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha kawaida cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kinachoanza leo.
Rais Kikwete anamaliza kipindi chake cha mwaka mmoja cha kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo na kumkabidhi uenyekiti kiongozi mwingine katika kikao hicho kama ilivyo katika taratibu za EAC.
Rais Kikwete alipokea uenyekiti kutoka kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda katika kikao cha Novemba mwaka jana.
Katika kikao cha wiki hii, viongozi watapokea taarifa mbalimbali za Baraza la Mawaziri zinazohusu utekelezaji wa masuala yanayohusu Jumuiya na kujadili mambo mbalimbali. |
|
No comments:
Post a Comment