MBUNGE wa Katavi, Mizengo Pinda amepitishwa kushika wadhifa wa uwaziri mkuu baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha kwa kura nyingi pendekezo la Rais Jakaya Kikwete jana. Uamuzi huo uliofanywa kwa kura za siri na wabunge 328 waliohudhuria kikao cha Bunge jana, unampa nafasi Pinda kushikilia nafasi hiyo kwa miaka takriban nane baada ya kuteuliwa Februari mwaka 2008 wakati Kikwete alipolazimika kuunda baraza jipya la mawaziri. Ukumbi wa Bunge ulilipuka kelele za shangwe mara baada ya Spika Anna Makinda kutaja jina la Pinda wakati akisoma barua ya Rais Kikwete. Wakati wabunge, hasa wa CCM wakipigapika meza kushangilia, Pinda alionekana kuwa mtulivu na mwenye kutafakari, akipepesa macho kulia na kushoto. Lakini sehemu ambayo walikaa wabunge wengi wa wapinzani na hasa Chadema, ambayo inaongoza kambi ya upinzani, hawakuonekana kushangilia na picha za televisheni ziliwaonyesha wakijadiliana mambo kana kwamba waligundua jambo ambalo halikwenda sawa. Baada ya Spika Makinda kusoma pendekezo hilo la Rais Kikwete, mwanasheria mkuu wa serikali, Frederick Werema alisimama na kutoa hoja ya kuliomba Bunge lithibitishe jina la waziri mkuu kwa mujibu kifungu cha 55 cha katiba. Mbali na kuelekeza utashi huo wa katiba, Werema alimwagia sifa Pinda kuwa ni mtu mpole, mwadilifu, asiyeyumbishwa, asiye na makuu na mwenye hekima, msikivu wa hali ya juu na mchapakazi. "Wabunge wote mtakubaliana nami kuwa anashaurika na anapokea ushauri kwa mikono miwili. Uwezo wake umejidhihirisha kwa muda mrefu na ana uwezo wa kuhimili wadhifa wa waziri mkuu," alisema Werema. Hoja yake iliungwa mkono na wabunge wa CCM ambao walisimama kwa pamoja mara baada ya Werema kuwasilisha hoja hiyo huku wakipiga makofi na wabunge wa upinzani wakiendelea kutulia kwenye viti. Wabunge wawili waliomba kuchangia hoja hiyo na Spika Makinda alimruhusu mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango kuwa wa kwanza kuchangia, lakini badala yake akaeleza kukubaliana na pendekezo hilo na kuomba hoja hiyo ipite bila ya kujadiliwa. "Namshukuru Mungu kwa kuwa ametutendea haki na rais amemteua mtu anayependwa na wengi. Naomba hoja hii ipite bila kujadiliwa," alisema Kilango. Mara baada ya kauli yake, wabunge wa CCM walisimama tena kuashiria kuunga mkono na Spika Sitta akasema hoja hiyo imepitishwa na hivyo kuelekea kwenye hatua nyingine ambayo ni kupiga kura ya siri kama ibara ya 51(1) inavyotaka. Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila ambaye alikuwa msimamizi wa zoezi la upigaji kura, alisema kuwa wabunge waliokuwemo ukumbini baada ya milango kufungwa walikuwa 327 lakini wakati akitangaza matokeo alisema kura zilizopigwa zilikuwa 328. Pinda alipata kura 277 za ndiyo ambazo ni sawa na asilimia 84.5, wakati za hapana zilikuwa 49 sawa na asilimia 4.9 na kura mbili ziliharibika ikiwa ni asilimia 0.6. Mawakala walioshuhudia uhesabuji wa kura za kuthibitishwa kwa Pinda ni Jenister Mhagama mbunge wa Peramiho CCM, David Kafulila mbunge wa Kigoma Kusini NCCR-Mageuzi na Tundu Lissu mbunge wa Singida Mashariki Chadema na Ibrahim Sanya wa CUF. Akizungumza baada ya kutangazwa kupitishwa, Pinda alishukuru kwa Rais Kikwete kuonyesha imani kwake na pia kwa Bunge kumpitisha, lakini akasema itakuwa vizuri zaidi kama chombo hicho kitajikita katika kuhakikisha kinaboresha maisha ya mkulima na mfugaji. "Ninapojiita mtoto wa mkulima, sitanii... naguswa na hali iliyopo vijijini kwa sababu watu walio huko ni wakulima na maskini," alisema Pinda. "Najua kuwa kutatokea kutoelewana, lakini kutoelewana huko hakutakuwa na maana kama hakutasaidia kuboresha maisha ya maskini." Akionekana kutambua kuwa wapinzani hawakufurahishwa na mambo yalivyoendelea, Pinda aliamua kueleza kilichokuwa moyoni. "Nilipata mashaka makubwa sana kutoka kwa ndugu zangu wa Chadema ambao walionyesha wazi tangu mwanzo kutopiga makofi, lakini katika hali kama hii huwa ni kitu cha kawaida wengine wanasema ndiyo na wengine kusema hapana ni hali ya kawaida lakini wote wametenda haki," alisema Pinda. "Siwezi kusema nimchukie (mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe au Khalifa Kisa kwa sababu wamenipigia kura za hapana, hapana, nitafanyakazi na pande zote mbili naombeni ushirikiano wenu." Pinda pia alimshukuru spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta kuwa aliweza kumsaidia kwa hali na mali katika kipindi chote cha utumishi wake na hali hiyo ililifanya Bunge kulipuka kwa makofi. Sitta alikuwepo bungeni wakati Pinda akisema hayo na picha za televisheni zilimuonyesha akitingisha kichwa kuashiria kukubaliana na maneno ya Pinda huku akimwaga tabasabu. Aliahidi pia kuboresha kipindi cha maswali ya papo kwa hapo na kwamba hatakuwa na shida katika kuyajibu, lakini akasisitiza kuwa angependa maswali hayo kutoka pande zote za vyama yalenge zaidi katika maslahi ya wananchi. Wakitoa maoni yao kuhusu uteuzi huo, watu walioongea na Mwananchi mkoani Dodoma walisema kuwa Rais Kikwete amekidhi utashi wa walio wengi kwa kumrejesha Pinda. Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idrisa Kikula amemuelezea Pinda kuwa ni mtu ambaye alimudu nafasi hiyo tangu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza Februari 2008 na kwamba kama mwingine angeteuliwa kusingekuwa na tija yoyote. "Kwa kweli uteuzi huu mimi binafsi haujanishtua kwa kuwa niliutarajia," alisema Prof Kikula. "Ingekuwa jambo la ajabu kabisa kama Kikwete angemuacha mtu anayeonekana wazi kuwa ni mwadilifu na mchapakazi kama huyu (Pinda) na kumteua mtu mwingine. “Ukimtazama, kwa kweli ni mtu ambaye hapigi makelele ovyo, yeye anachapa kazi na kutimiza wajibu wake taratibu kwa umakini mkubwa na uhakika, hivyo kusingekuwa na haja ya uteuzi wa mtu mwingine.” Lakini alimtaka Pinda kuwa makini kwa kuwa kipindi hiki Bunge lina idadi kubwa ya wabunge wa upinzani kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi. Naye Daudi Nyinge, ambaye kitaaluma ni mwalimu, aliusifu uteuzi huo lakini akamtaka Pinda kuhakikisha anatekeleza wajibu wake bila kuingiza itikadi za kichama. Alisema kwa namna yoyote asiwachukie wapinzani bali ajishughulishe na utatuzi wa kero za wananchi akieleza kuwa mtaji wa wapinzani ni hizo kero. Chanzo : Mwananchi. |
Wednesday, November 17, 2010
Pinda awa Waziri Mkuu tena
Labels:
uchaguz2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment