MBUNGE wa Katavi, Mizengo Pinda amepitishwa kushika wadhifa wa uwaziri mkuu baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha kwa kura nyingi pendekezo la Rais Jakaya Kikwete jana. Uamuzi huo uliofanywa kwa kura za siri na wabunge 328 waliohudhuria kikao cha Bunge jana, unampa nafasi Pinda kushikilia nafasi hiyo kwa miaka takriban nane baada ya kuteuliwa Februari mwaka 2008 wakati Kikwete alipolazimika kuunda baraza jipya la mawaziri. Ukumbi wa Bunge ulilipuka kelele za shangwe mara baada ya Spika Anna Makinda kutaja jina la Pinda wakati akisoma barua ya Rais Kikwete. Wakati wabunge, hasa wa CCM wakipigapika meza kushangilia, Pinda alionekana kuwa mtulivu na mwenye kutafakari, akipepesa macho kulia na kushoto. Lakini sehemu ambayo walikaa wabunge wengi wa wapinzani na hasa Chadema, ambayo inaongoza kambi ya upinzani, hawakuonekana kushangilia na picha za televisheni ziliwaonyesha wakijadiliana mambo kana kwamba waligundua jambo ambalo halikwenda sawa. Baada ya Spika Makinda kusoma pendekezo hilo la Rais Kikwete, mwanasheria mkuu wa serikali, Frederick Werema alisimama na kutoa hoja ya kuliomba Bunge lithibitishe jina la waziri mkuu kwa mujibu kifungu cha 55 cha katiba. Mbali na kuelekeza utashi huo wa katiba, Werema alimwagia sifa Pinda kuwa ni mtu mpole, mwadilifu, asiyeyumbishwa, asiye na makuu na mwenye hekima, msikivu wa hali ya juu na mchapakazi. "Wabunge wote mtakubaliana nami kuwa anashaurika na anapokea ushauri kwa mikono miwili. Uwezo wake umejidhihirisha kwa muda mrefu na ana uwezo wa kuhimili wadhifa wa waziri mkuu," alisema Werema. Hoja yake iliungwa mkono na wabunge wa CCM ambao walisimama kwa pamoja mara baada ya Werema kuwasilisha hoja hiyo huku wakipiga makofi na wabunge wa upinzani wakiendelea kutulia kwenye viti. Wabunge wawili waliomba kuchangia hoja hiyo na Spika Makinda alimruhusu mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango kuwa wa kwanza kuchangia, lakini badala yake akaeleza kukubaliana na pendekezo hilo na kuomba hoja hiyo ipite bila ya kujadiliwa. "Namshukuru Mungu kwa kuwa ametutendea haki na rais amemteua mtu anayependwa na wengi. Naomba hoja hii ipite bila kujadiliwa," alisema Kilango. Mara baada ya kauli yake, wabunge wa CCM walisimama tena kuashiria kuunga mkono na Spika Sitta akasema hoja hiyo imepitishwa na hivyo kuelekea kwenye hatua nyingine ambayo ni kupiga kura ya siri kama ibara ya 51(1) inavyotaka. Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila ambaye alikuwa msimamizi wa zoezi la upigaji kura, alisema kuwa wabunge waliokuwemo ukumbini baada ya milango kufungwa walikuwa 327 lakini wakati akitangaza matokeo alisema kura zilizopigwa zilikuwa 328. Pinda alipata kura 277 za ndiyo ambazo ni sawa na asilimia 84.5, wakati za hapana zilikuwa 49 sawa na asilimia 4.9 na kura mbili ziliharibika ikiwa ni asilimia 0.6. Mawakala walioshuhudia uhesabuji wa kura za kuthibitishwa kwa Pinda ni Jenister Mhagama mbunge wa Peramiho CCM, David Kafulila mbunge wa Kigoma Kusini NCCR-Mageuzi na Tundu Lissu mbunge wa Singida Mashariki Chadema na Ibrahim Sanya wa CUF. Akizungumza baada ya kutangazwa kupitishwa, Pinda alishukuru kwa Rais Kikwete kuonyesha imani kwake na pia kwa Bunge kumpitisha, lakini akasema itakuwa vizuri zaidi kama chombo hicho kitajikita katika kuhakikisha kinaboresha maisha ya mkulima na mfugaji. "Ninapojiita mtoto wa mkulima, sitanii... naguswa na hali iliyopo vijijini kwa sababu watu walio huko ni wakulima na maskini," alisema Pinda. "Najua kuwa kutatokea kutoelewana, lakini kutoelewana huko hakutakuwa na maana kama hakutasaidia kuboresha maisha ya maskini." Akionekana kutambua kuwa wapinzani hawakufurahishwa na mambo yalivyoendelea, Pinda aliamua kueleza kilichokuwa moyoni. "Nilipata mashaka makubwa sana kutoka kwa ndugu zangu wa Chadema ambao walionyesha wazi tangu mwanzo kutopiga makofi, lakini katika hali kama hii huwa ni kitu cha kawaida wengine wanasema ndiyo na wengine kusema hapana ni hali ya kawaida lakini wote wametenda haki," alisema Pinda. "Siwezi kusema nimchukie (mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe au Khalifa Kisa kwa sababu wamenipigia kura za hapana, hapana, nitafanyakazi na pande zote mbili naombeni ushirikiano wenu." Pinda pia alimshukuru spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta kuwa aliweza kumsaidia kwa hali na mali katika kipindi chote cha utumishi wake na hali hiyo ililifanya Bunge kulipuka kwa makofi. Sitta alikuwepo bungeni wakati Pinda akisema hayo na picha za televisheni zilimuonyesha akitingisha kichwa kuashiria kukubaliana na maneno ya Pinda huku akimwaga tabasabu. Aliahidi pia kuboresha kipindi cha maswali ya papo kwa hapo na kwamba hatakuwa na shida katika kuyajibu, lakini akasisitiza kuwa angependa maswali hayo kutoka pande zote za vyama yalenge zaidi katika maslahi ya wananchi. Wakitoa maoni yao kuhusu uteuzi huo, watu walioongea na Mwananchi mkoani Dodoma walisema kuwa Rais Kikwete amekidhi utashi wa walio wengi kwa kumrejesha Pinda. Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idrisa Kikula amemuelezea Pinda kuwa ni mtu ambaye alimudu nafasi hiyo tangu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza Februari 2008 na kwamba kama mwingine angeteuliwa kusingekuwa na tija yoyote. "Kwa kweli uteuzi huu mimi binafsi haujanishtua kwa kuwa niliutarajia," alisema Prof Kikula. "Ingekuwa jambo la ajabu kabisa kama Kikwete angemuacha mtu anayeonekana wazi kuwa ni mwadilifu na mchapakazi kama huyu (Pinda) na kumteua mtu mwingine. “Ukimtazama, kwa kweli ni mtu ambaye hapigi makelele ovyo, yeye anachapa kazi na kutimiza wajibu wake taratibu kwa umakini mkubwa na uhakika, hivyo kusingekuwa na haja ya uteuzi wa mtu mwingine.” Lakini alimtaka Pinda kuwa makini kwa kuwa kipindi hiki Bunge lina idadi kubwa ya wabunge wa upinzani kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi. Naye Daudi Nyinge, ambaye kitaaluma ni mwalimu, aliusifu uteuzi huo lakini akamtaka Pinda kuhakikisha anatekeleza wajibu wake bila kuingiza itikadi za kichama. Alisema kwa namna yoyote asiwachukie wapinzani bali ajishughulishe na utatuzi wa kero za wananchi akieleza kuwa mtaji wa wapinzani ni hizo kero. Chanzo : Mwananchi. |
Showing posts with label uchaguz2010. Show all posts
Showing posts with label uchaguz2010. Show all posts
Wednesday, November 17, 2010
Pinda awa Waziri Mkuu tena
Sunday, November 7, 2010
KIKWETE AAPISHWA KUWA RAISI
Raisi mteule Jakaya Mrisho Kikwete akiapa kwa kushika kitabu kitakatifu (TheHolly Qur'an ) mbele ya Jaji mkuu wa Tanzania Jaji Agustino Ramadhani.
Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameapishwa baada ya kushinda matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010.
Rais ameapa mbele ya jopo la viongozi wa serikali wakiwemo Jaji Mkuu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi, Jopo la Majaji, Wakuu wa Vyombo vya ulinzi, Viongozi Watatu wa Madhehebu ya Dini, Wazee Wawili kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani na Karani wa Baraza la Mawaziri.
Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameapishwa baada ya kushinda matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010.
Rais ameapa mbele ya jopo la viongozi wa serikali wakiwemo Jaji Mkuu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi, Jopo la Majaji, Wakuu wa Vyombo vya ulinzi, Viongozi Watatu wa Madhehebu ya Dini, Wazee Wawili kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani na Karani wa Baraza la Mawaziri.
| Raisi Jacob Zuma wa Africa ya kusini Sherehe hizi zimehudhuriwa na marais 5 wa nchi za Afrika akiwemo Robert Mugabe wa Zimbabwe, Mwai Kibaki wa Kenya, Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini, Rupia Banda wa Zambia na Joseph Kabila wa DRC. Raisi Mwai Kibaki wa kenya Raisi Robert Mugabe wa Zimbabwe |
KIKWETE ASHINDA URAISI KWA 61.7%
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza Kikwete aliyekuwa akigombea nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM, kuwa mshindi baada ya kupata kura 5,276,827 (sawa na 61.17%) ya kura zote halali zilizopigwa 8,626,283.
Akitangaza matokeo hayo Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Lewis Makame, alisema Kikwete alipata ushindi huo, miongoni mwa wagombea wa vyama saba vya siasa waliowania.
Aliyekuwa mgombea wa Chadema, Dk Willibrod Slaa hakuhudhuria hafla hiyo kutokana na kile alichodai juzi kuwa hakubaliani na matokeo.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, nafasi ya pili katika kinyang’anyiro hicho ilichukuliwa na Willibrod Slaa wa Chadema ambaye alipata kura 2,271,941 (sawa na 26.34%) ya kura zote halali.
Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 695,667 (sawa na 8.06% ) ya kura zote halali.
Baada ya kutangaza matokeo hayo, Rais Kikwete aliwashukuru wapiga kura, NEC na vyombo vya habari kwa kuwezesha uchaguzi huo kufanyika kwa utulivu na amani.
Alisema, “ushindi niliopata unaonesha imani ya wapiga kura kwangu na ninaahidi nitawatumikia kwa ari mpya zaidi, nguvu mpya zaidi na kasi mpya zaidi.” .
Thursday, November 4, 2010
Dr Slaa : Matokeo yamechakachuliwa...
Dk Willibrod Slaa.
Kauli hiyo imetolewa wakati Tume ya Uchaguzi (Nec) ikielekea kukamilisha kutangaza matokeo ya majimbo na kumtangaza mshindi, jambo ambalo litamfanya Dk Slaa na chama chake kuzuiwa na katiba ya nchi kupinga matokeo hayo mahakamani.
Dk Slaa aliwaambia waandishi wa habari jana akisema kuwa: "Kuna uchakachuaji mkubwa wa kura na kazi hiyo inafanywa na Usalama wa Taifa," alisema Dk Slaa ambaye matokeo yanayotangazwa na Nec yanaonyesha kuwa anaendelea kushika nafasi ya pili akiwa nyuma ya mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
Lakini Mwenyekiti wa Nec, Jaji Lewis Makame alipoulizwa kuhusu tamko hilo la Chadema, alimtaka Dk Slaa kuwasilisha taarifa zinazothibitisha madai aliyoyatoa kuwa Nec imekuwa ikitangaza matokeo yaliyochakachuliwa tofauti na zile alizopata.
Jaji Makame alisema kama madai ya Dk Slaa ni ya kweli, ni muhimu apeleke hizo idadi ya kura alizodai amepunjwa ili kuthibitisha madai yake dhidi ya tume hiyo.
Alisema idadi ya kura zinazotangazwa na Nec kwenye kinyang’anyiro cha urais ni zile ambazo wagombea hao wamezipata kihalali kwenye upigaji kura na wala hakuna upendeleo wowote.
“Mimi sijapata malalamiko yoyote kutoka kwa mgombea huyo, hivyo kama anayoyazungumza ni ya kweli kuna umuhimu wa kuthibitisha hiyo tofautu anayodai ipo, lakini kura tunazotangaza ni kura ambazo kila mgombea alizipata kwenye uchaguzi," alisema Jaji Makame
Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Karatu alionya kama Nec inaitakia mema nchi hii, ifute matokeo yote ya urais na uchaguzi urudiwe upya.
"Hatuwezi kukubali matokeo yanayopikwa na Usalama wa Taifa. Hayo si matakwa ya wananchi," alisema Dk Slaa baadaye kukaririwa kwenye TBC.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, ambaye pia ni katibu mkuu wa Chadema, chama chake kimekuwa kikifuatilia kwa makini matokeo hayo na kugundua wizi mkubwa wa kura kwenye nafasi za urais na ubunge.
Mgombea huyo wa urais, ambaye mara nyingi hujenga hoja kwa kutumia ushahidi, alisema moja ya maeneo waliyogundua kuwepo kwa wizi wa kura ni matokeo ya Jimbo la Geita lililo mkoani Mwanza ambako alidai Nec ilitangaza kuwa kwenye uchaguzi wa rais, CCM imepata kura 17,792 na Chadema kura 3,789.
Lakini akasema kwa mujibu wa fomu walizonazo ambazo zilisainiwa na mawakala wao kwenye kata 20 za jimbo hilo, CCM ilipata kura 30,960 na Chadema 15,736.
"Nashangaa Nec wanatangaza matokeo haya kutoka wapi? Hayo ya Geita ni moja tu. Kule Hai, fomu zinaonyesha kwenye urais CCM ina kura 20,120 na Chadema 26,724, lakini Nec imetangaza kuwa CCM ina kura 35,910 na Chadema kura 18,513," alisema Dk Slaa huku akionyesha baadhi ya fomu kwa waandishi wa habari.
Dk Slaa pia alitoa mfano aliodai kuwa wizi wa kura katika kituo namba 00070103 cha Ubungo jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa fomu 24A inaonyesha CCM wamepata kura 68,727 na Chadema 65,450, lakini matokeo ya kata za Ubungo yanaonyesha CCM ina kura 70,472 na Chadema 72,252.
Dk Slaa alisema mbali na Ubungo, tatizo hilo pia alidai liko Kigoma Mjini ambako Chadema imeshinda kwa zaidi ya kura 500, lakini "matokeo yalichakachuliwa na kusababisha vurugu hadi askari wakawapiga mabomu wafuasi wa Chadema".
Pia alisema kwenye Jimbo la Segerea, ambako matokeo yalicheleweshwa kwa siku mbili na kutangazwa usiku wa manane juzi, mambo ni mabaya zaidi kwa kuwa fomu 21 A na B hazikuwepo na wasimamizi walikwenda nazo majumbani kulala.
"Kiwalani fomu hazikuwepo na matokeo hayakuonekana. Kipawa vituo vinne matokeo hayakuonekana na Vingunguti kuna vituo saba na Tabata vituo viwili ambako matokeo hayakuonekana," alisema Dk Slaa.
Aliongeza kusema: "Hali kama hiyo pia imetokea Morogoro Mjini. Matokeo hayajaonekana na yametangazwa tu. Kibakwe na Kiteto mgombea hakushirikishwa katika kutangaza matokeo.
"Hayo ni majimbo ya mifano tu. Yapo majimbo mengi na kutokana na hali hiyo, Chadema imetoa tahadhari kwa Tume na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa taratibu hazijafuatwa na nyingi zimevunjwa."
Dk Slaa alisema kuwa ni muhimu waangalizi wote wa uchaguzi wakatoa taarifa zao hadharani ili kusaidia nchi na kumtaka mkuu wa Jeshi la Polisi kuendesha chombo hicho cha dola kwa haki na maadili waliyosaini.
Baadaye mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa kauli hiyo ya Dk Slaa ni tamko rasmi la Chadema.
Akizunguzia ucheleweshaji wa mataokeo unaodaiwa kutokea kwenye majimbo ambayo CCM imeonekana kukabwa koo na vyama vyama vya upinzini, Jaji Makame alisema wao wanatangaza matokea wanayopelekewa na wala hakuna ucheleweshaji wowote.
Mkuu wa kitengo cha uchaguzi cha CCM, Mattson Chizi alisema hoja za Dk Slaa zimejikita kwenye matokeo yanayotangazwa na Nec hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo.
"Tunachosubiria ni matokeo ya jumla na hatuwezi kuingilia kazi ya tume," alisema.
Kwa upande wa CUF, Meneja wa Kampeni wa chama hicho, Said Miraji, alisema aligoma kuzungumzia suala akieleza kwamba CUF kitaandaa taarifa kuhusu uchaguzi ambayo itatolewa baadaye na mgombea urais wao, Prof Ibrahim Lipumba.
CHANZO: MWANANCHI
Subscribe to:
Posts (Atom)
