Home

HOME I

Saturday, September 18, 2010

Wizi wa vifaa katika magari kutoka nje wakithiri

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania( TPA), imesema asilimia 80 ya magari yanaoibwa vifaa vinaibwa kabla ya kuingia katika bandari ya Dar es Salaam.

Jana waandishi wa habari walikuwa watu kwanza kukagua magari yaliyoletwa katika meli kabla ya wafanyakazi wa bandari kuingia ndani na kushuhudia magari mengi yakiwa yameibiwa redio na vifaa vya kufungulia madirisha.

Takwimu zinaonyesha magari mengi yanaibiwa vifaa katika bandari ya Sharjah, Falme za Kiarabu na yanayotokea Japan yana usalama zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua meli iliyobeba magari hayo, Meneja wa bandari ya Dar es Salaam, Idi Mkwata alisema, vifaa vya magari hayo vinaibwa katika maeneo makuu manne ambayo ni kabla ya magari hajapakiwa melini kuja nchini na magari yakiwa melini wakati yanakuja Dar es Salaam.

Pia yanaibwa vifaa magari yakiwa bandarini na wakati yakiwa mikononi mwa mawakala wasio waaminifu yakipelekwa kwa wenye magari.

Katika kipindi cha kati ya Januari na Agosti mwaka huu kati ya magari yaliyofika 36,708, magari 31,794 yaliibwa vifaa na magari 4,914 yalikutwa na vifaa kamili huku 39 ndiyo yalifanyiwa uharibifu yakiwa ndani ya bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mwaka jana kati ya magari yaliyoingia 52,411 magari 39,780 yalikutwa yameshanyofolewa vifaa kabla ya kuteremshwa na 12,631 yalikutwa na vifaa kamili huku 71 yaliibwa vifaa yakiwa ndani ya bandari ya Dar es Salaam.

Mkuu wa Usalama wa TPA, David Mranda alisema, magari yanapobainika kuibwa vifaa vyake kabla ya kushushwa katika bandari ya Dar es Salaam, uongozi wa bandari unatoa taarifa kwa Mkuu wa meli ambaye anawasilisha malalamiko katika eneo alipochukua gari lakini yanayoibwa ndani ya bandari TPA ndiyo inayomlipa mtu fidia.

Katika kukabiliana na wizi huo, TPA kwa kushirikiana na uongozi wa bandari ya Sharjah umeanzisha fomu ya ukaguzi wa magari yanapopakiwa Sharjah ili kubaini yote yaliyofanyiwa uharibifu yakiwa huko, utaratibu umeanza kupunguza wizi huo.

“Hatua tulizochukua katika bandari ya Dar es Salaam ni matumizi ya mtandao wa kamera za kiusalama(CCTV) katika yadi za magari; kuweka uzio kwenye yadi na kuzuia wateja na watu wengine kuingia katika yadi za magari kiholela”, alisema Mranda.

Hatua nyingine ni matumizi ya ving’amuzi vya metali; kukagua magari kwenye meli kabla ya hayajateremshwa kutoka melini na matumizi ya fomu za kukagulia magari(VDITT) ambayo inatakiwa kubandikwa kwenye gari ili mmiliki wa gari aweze kutambua vifaa vilivyopo ndani ya gari yake.

Kwa sasa bandari ina uwezo wa kuhifadhi magari 3,600 katika eneo la bandari na yadi ya nje ya magari ina uwezo wa kuhifadhi magari 1,500 kwa wakati mmoja.

Alisema, wiki ijayo yadi nyingine yenye uwezo wa kuhifadhi magari 1,500 itafunguliwa na Oktoba yadi nyingine ya nje ya kuhifadhi magari 2,500 itaanza kutumika.