Home

HOME I

Wednesday, October 13, 2010

Samuel Sitta anatisha

*Ahamishia Ofisi ya Spika wa Bunge Urambo Mashariki
*Thamani yake yamduwaza Kikwete, asema nchi itafilisika.

MBUNGE wa Urambo Mashariki, mkoani Tabora, Samuel Sitta, amedhihirisha kwamba yeye ni mtu wa viwango vya hali ya juu, baada ya kuomba Serikali imjengee Ofisi ya Jimbo, yenye hadhi sawa na Ofisi ya Spika iliyoko katika jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyoko Dodoma.

Ofisi hiyo, ambayo ilizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita, inaelezwa kuigharimu Serikali zaidi ya Sh milioni 500, kama zitajumlishwa gharama za ujenzi pamoja na samani (furniture) zilizomo ndani ya ofisi hiyo, maalumu kwa ajili ya mbunge wa jimbo la Urambo Mashariki.

Haikuweza kufahamika ni kwanini Sitta, ambaye pia ni Spika wa Bunge linalomaliza muda wake, aliamua kujenga ofisi mpya wakati tayari anayo Ofisi ya Mbunge katika jengo la mkuu wa wilaya ya Urambo.

Rai limeelezwa kwamba kila mbunge, katika mwaka wa fedha wa 2009/2010, alitengewa  Sh milioni 65 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya mbunge jimboni kwake, lakini mbunge wa Urambo Mashariki yeye aliamua ajenge ofisi yenye hadhi ya nafasi yake ya Uspika.

Habari zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya watu walioshuhudia hafla ya uzinduzi wa ofisi hiyo uliofanywa na Rais Kikwete wiki iliyopita, zinasema hata Rais alishitushwa na hadhi ya ofisi hiyo, kiasi cha kujikuta akitamka kwamba ‘kama kila mbunge atataka ajengewe ofisi ya kiwango hiki, basi wabunge wataifilisi nchi hii.’

Jengo la ofisi hiyo ya jimbo, mbali na kuwa na ofisi ya mbunge, inayo pia ofisi ya msaidizi wa mbunge, katibu muhtasi, watumishi wengine wasaidizi (technical staff), chumba maalumu cha watu mashuhuri (vip lounge) na ukumbi wa mikutano unaoweza kuwakusanya watu 30 wakiwa wamekaa kwenye viti.

Rai limefanikiwa kupata baadhi ya nyaraka za mawasiliano baina ya Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhani Khijjah, zinazoelezea uhamishwaji wa fedha kutoka katika vifungu vya maendeleo (fungu 42) kwenda fungu Na 85 cha RAS Tabora ili zikafanye kazi ya ujenzi wa ofisi hiyo.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Juni 11 mwaka jana, Dk Kashililah alimwandikia barua Khijjah, akijibu barua ya Katibu Mkuu huyo yenye kumb. Na. C/AB/422/01 ya Mei 13, 2009, ambayo ilielekeza kutenga fedha kwenye Fungu 42: Mfuko wa Bunge, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa ofisi ya mbunge wa Urambo Mashariki.

Katika barua hiyo, Dk Kashililah anamuomba Katibu Mkuu Hazina, kuhamisha Sh milioni 200 kutoka Fungu 42 kwenda Fungu 85: Mkoa wa Tabora “kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya mbunge wa jimbo la Urambo Mashariki.”

Kwa mujibu wa barua hiyo, fedha hizo ziliombwa ‘kwa ajili ya kukamilisha ujenzi’ na si kuanza ujenzi, hali inayotafisiriwa na wachambuzi wa mambo ya ujenzi kwamba wakati kiasi hicho cha fedha kikiombwa, tayari mradi huo ulikwishatumia kiasi kingine zaidi ya hicho, kuanzia ujenzi wenyewe, usanifu na uchoraji wa ramani ya jengo.

Pamoja na barua hiyo, ipo barua nyingine ya Juni 4, mwaka huu, ambayo Katibu wa Bunge, Dk Kashililah alimwandikia Katibu Mkuu Hazina, akiomba kuhamishwa Sh milioni 72 kutoka katika fungu hilo la 42 kwenda fungu 85 kwa ajili pia ya ‘kukamilisha ujenzi wa ofisi ya mbunge wa Urambo Mashariki.

“Mradi huo (ofisi ya mbunge wa Urambo Mashariki) haukuweza kukamilika kutokana na upungufu wa fedha zilizopelekwa kupitia Fungu 85: RAS Tabora. Ili kuweza kukamilisha kazi hiyo, naomba kuhamisha kiasi cha Sh 72,000,000 kutoka Fungu 42: Mfuko wa Bunge kwenda Fungu 85: RAS Tabora. Fedha hizo (Sh milioni 72) zihamishwe kutoka vifungu vya maendeleo ambazo hazikuweza kutolewa kutokana na kuchelewa kutekelezwa kwa miradi iliyokusudiwa,” inasema sehemu ya barua hiyo ya Dk Kashililah.

Dk Kashililah amekiri kuwapo kwa mawasiliano hayo baina yake na Katibu Mkuu wa Hazina pamoja na uhamishaji wa fedha hizo kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Bunge ili zikatumike kujenga ofisi hiyo, akisema mradi huo ni sehemu ya miradi ya maendeleo ya Bunge.

Juhudi za kumpata Katibu Mkuu Hazina jana hazikufanikiwa baada ya mtu mmoja katika ofisi yake, aliyejitambulisha kuwa Katibu Muhtasi wake, kuliambia Rai kwamba Katibu huyo, kwa wakati huo tuliopiga simu, alikuwa Ikulu.

Mbali na mamilioni hayo ya Shilingi yaliyotumika katika ujenzi wa ofisi ya mbunge huyo, samani za ofisi (furniture) zilizonunuliwa kwa ajili ya matumizi ya ofisi, zimeigharimu Serikali Sh 100,931,300.00.

Msambazaji wa samani hizo, ambaye alipatikana kwa utaratibu wa wazi kabisa wa zabuni ni M/S Mariedo Home Decor. Huyo naye anatiliwa shaka na baadhi ya wadadisi wa mambo, akidaiwa kuwa mshirika wa karibu wa mbunge wa Urambo Mashariki.

Shaka hiyo, inatokana na ukweli kwamba katika wazabuni wanne waliokuwa wameorodheshwa na Bodi ya Zabuni ya Bunge, M/S Meriedo ndiye aliyekuwa mtu ghali sana, pengine mara mbili ya wengine.

Kwa mujibu wa fomu ya ulinganisho wa bei za Wazabuni (Comparison of Technical Aspects Against Quoted Price), Wazabuni wanne waliokuwa wameteuliwa, bei zao zikiwa katika mabano, ni pamoja na M/S Living Room (Sh 64,769,960.00), M/S Quality Furniture and General Appliance (Sh 49,967,760.00), M/S Mariedo Home Décor (Sh 100,931,300.00 na M/S Alea Industries Ltd (80,462,624.00).

Miongoni mwa mahitaji muhimu katika ofisi ya mbunge huyo, ambayo yanalazimika kununuliwa na Serikali, ni pamoja na kompyuta ndogo (Laptop) ya inchi 17, mashine ya kudurufu karatasi (printer), Televisheni kubwa na ungo wake (Flat Screen TV with Dish), kioo kikubwa na vidude vya kutundikia koti ofisini (Coat hanger).

Aidha, kwenye korido ya kuingilia ofisini kwake, inahitajika seti moja ya viti vya bustanini, stuli 4 na meza ndogo ya bustanini, wakati ukumbi wa mikutano unahitaji kuwekewa meza ya mikutano na viti 24, huku vikihitajika pia viti vya dharura sita pamoja na dawati dogo moja.

Katika moja ya madokezo kati ya Mkurugenzi wa Utawala wa Wilaya ya Urambo (DAD) na wataalamu wake, katika kujadili aina ya samani na gharama zake zinazohitajika kununuliwa kwa ajili ya ofisi hiyo, imeandikwa:

“Baada ya kushirikiana na Msaidizi wa Spika, na kutokana na ‘taste’ ya Mh Spika, gharama ya ununuzi wa samani ni Sh 69,560,000.00 kutoka kwa M/S Mariedo Home Décor. Gharama hizi hazihusishi items zifuatazo: Air Condition, Laptop, kompyuta, photocopy mashine, Fax Machine, Printer na Generator ya 20kv.”

Ofisi hiyo ya mbunge wa Urambo Mashariki, ilizinduliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete, siku chache baada ya kuhutubia Bunge na kuahirishwa, kabla ya kuvunjwa rasmi Agosti Mosi mwaka huu.

Watanzania walio wengi, walioshuhudia hafla ya ufunguzi huo kwa macho na au kupitia matangazo ya vituo vya televisheni nchini, walionyeshwa kushitushwa na ukubwa na ubora wa ofisi hiyo, kiasi cha baadhi ya watazamaji hao kupiga simu chumba cha habari cha gazeti hili, wakisema: “Kumbe Serikali hii ina fedha nyingi, haiwezekani ofisi ya mbunge ifanane na ukumbi wa Bunge Dodoma.”

Wengine walikwenda mbele zaidi na kuhoji: “Kwa nini mbunge, na hasa majimbo ya Urambo awe na ofisi ya gharama kubwa ya namna ile wakati wakazi wa Urambo ni masikini wa kutupwa ikilinganishwa na wilaya nyingine nchini?”

No comments: