Home

HOME I

Sunday, November 7, 2010

Mashoga Ruksa kuwa Wanajeshi Marekani

JESHI la Marekani limekubali kuanza kutoa mafunzo ya kijeshi kwa mashoga baada ya wiki iliyopita Jaji wa Jimbo la California kutengua sera ya 'usiulize, usimwambie'. Sera hiyo ilikuwa ikipinga wazi mashoga kutumikia jeshi ingawa Wizara ya Ulinzi imewaonya wanajeshi mashoga ikisema kuwa huenda sheria hiyo ikatenguliwa.

Habari kutoka mjini Washington DC zimeeleza kuwa, pamoja na sera hiyo ya kupinga mashoga kutumikia jeshi kutenguliwa, Pentagon imekata rufaa kuhusu uamuzi huo na kumtaka Jaji kurejesha kwa muda sera hiyo lakini Jaji Virginia Phillips jana alikataa ombi hilo.

Imeelezwa kuwa baada ya kuondolewa sera hiyo, makundi ya wanaharakati wa kutetea haki za mashoga wamepanga kupeleka watu wa jamii hiyo kwenye vituo vya mafunzo ya kijeshi ili kujaribu tamko hilo la Pentagon.

"Endapo wenyewe binafsi watakubali wazi kuwa ni mashoga na wanataka kujifunza jeshi, tutawafanyia utaratibu lakini tutawaeleza kuwa hali hiyo kisheria inaweza kubadilika," amesema msemaji wa Idara ya Mafunzo ya Kijeshi katika kituo cha Fort Knox, Kentucky, Douglas Smith.

Mwezi Septemba mwaka huu, Chama cha Democrats kilijaribu kuitengua sera hiyo ya kuzuia mashoga kutumikia jesheni kupitia Baraza la Seneti lakini kikashindwa baada ya kushindwa kupata kura za kutosha.

Naye Rais Barack Obama, alishatangaza kuiondoa sera hiyo lakini wengi wa washauri wake wanakubali kuwa Rais huyo hawezi kuondoa sera hiyo ya kuwapiga marufuku mashoga kutumikia wazi jeshini bila kupitishwa na Baraza la Congress ama hatua za kisheria.

Katika hatua nyingine, Pentagon imesema kuwa Desemba mosi mwaka huu, inatarajia kutoa taarifa kuhusu uwezekano wa kuwepo madhara watakapowaruhusu wazi mashoga kutumikia jeshini.

Baadhi ya maofisa wa Pentagon wanasema kuwa kuwaruhusu mashoga kutaleta mabadiliko ya kila kitu jeshini kuanzia nyumba, bima na itifaki katika shughuli za kijamii.

Mjini California, Jaji Phillips anadai kuwa sera hizo zinavuruga haki za wanajeshi mashoga kuwa huru kuzungumza na kupata ulinzi sawa chini ya sheria.

Kesi ya kupinga kuzuiwa mashoga jeshini ilifunguliwa na kundi kutoka chama cha Republicans kinachounga mkono mashoga kwa niaba ya wanajeshi mashoga ambao walitimuliwa.


                                            Source: DarLeo

No comments: