Home

HOME I

Monday, November 1, 2010

Masha, Batilda, Mramba, Mkuchika mambo magumu

 
Mwenendo wa matokeo ya awali yaliyokuwa yakikusanywa hadi jana usiku yameonyesha kuwa vigogo takribani wagombea 10 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wana hali ngumu.Taarifa zilizokusanywa na Mwananchi katika majimbo mbalimbali zinaonyesha kuwa Philip Marmo (Mbulu), Lawrance Masha (Nyamagana), Dk Batilda Buriani (Arusha Mjini), Kapteni George Mkuchika (Newala) na Basil Mramba (Rombo) hali zao ni ngumu katika uchaguzi huu.

Matokeo yalikusanywa katika kata za majimbo ya wagombea hao yanaonyesha kwamba kuna mchuano mkali sana baina yao na wale wa vyama vingine na baadhi yao wamezidiwa hadi zaidi ya nusu ya kura, huku kata zilizobaki katika majimbo hayo zikiwa ni za kunyang'anyana.

Washindani wakubwa wa wagombea hao wanatoka CHADEMA na CUF ambavyo vimeweza kuongeza ushawishi katika maeneo mbalimbali nchini, kubwa ikiwa ahadi yao ya kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita.

Hadi jana jioni mvutano ulikuwa mkali katika majimbo hayo huku askari wa jeshi na wale wa polisi wakijaribu kutuliza hali ya mvutano uliokuwa umeanza kujikita kwenye majimbo hayo.

Taarifa zaidi zilieleza ukiukwaji wa taratibu wakati wa kura za maoni, tuhuma za rushwa na wanachama kupinga maamuzi ya baadhi ya kamati za siasa za mikoa kugeuza matokeo, ni mambo ambayo yanaendelea kuisumbua CCM.

Matokeo mengine ya awali ya urais, ubunge na udiwani yalionyesha jimbo la Simanjiro Kata ya Ngorika kura za urais CCM imepata kura 853, CHADEMA 282, CUF 5, APPT 3 na NCCR 1. Udiwani katika Kata hiyo CCM imepata kura 941 na CHADEMA 200.

Katika Kata ya Kibaya jimbo la Kiteto, kura za urais CCM imepata 83, CHADEMA 102 na CUF kura 4. Katika ubunge CHADEMA imepata kura 132, CCM 60 na CUF 2. Kwa upande wa udiwani CHADEMA imepata kura 125 na CCM 67.

Katika Kata ya Sanya Juu jimbo la Siha CCM imepata 1,269 na CHADEMA 949.

Kata ya Ngamiani Kusini, urais APPT 3, CCM 1,145, CHADEMA 104, CUF 1,254 na NCCR 4 udiwani CCM 11,180, CHADEMA 52, CUF 1,479 na UDP 5. Ubunge  jimbo la Lupa, CCM 1,039, TLP 589, CHADEMA 37 na CUF 5.

Source: Mwananchi

No comments: